Lugha Nyingine
Kujifunza kwa kufanya vitendo kwawaandaa watoto wa Tanzania kwa ajili ya siku zijazo (2)
![]() |
| Wanafunzi wakijifunza ujuzi wa msingi wa umeme kwenye darasa la ujuzi wa vitendo katika Shule ya Awali na Msingi ya De'kayra, Bagamoyo, Tanzania, Agosti 7, 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman) |
DAR ES SALAAM - Kwenye shule ya msingi katika mji wa pwani wa Bagamoyo nchini Tanzania, watoto wanajifunza kutazama zaidi ya vitabu vya kiada na mitihani, wakijenga ujuzi wa vitendo tangu umri mdogo ili kuwasaidia kujiandaa kwa ajili ya siku zijazo.
"Siku za baadaye za dunia ziko katika chumba hiki," yanasomeka maandishi ya kukolezwa ukutani mwa darasa kwenye Shule ya Awali na Msingi ya De'kayra. Ndani ya darasa hilo lenye mwanga angavu, ujumbe huo tayari unaanza kuwa hali halisi.
Wanafunzi wa miaka mitano Lightness Peter na Careen Aggrey walisimama kwa ujasiri mbele ya kompyuta ya mezani, wakionyesha sehemu za msingi za kompyuta hizi, ikiwemo monita, kibodi na kitengo cha kati cha kuchakata mifumo, na kuelezea namna zinavyofanya kazi pamoja.
"Lengo langu ni kuwa fundi wa kompyuta aliyebobea kikamilifu katika siku zijazo," Peter anasema huku akitabasamu.
Ndani ya darasa lingine, Brainier Lambert, mwenye umri wa miaka 10, na Judith Mwaria, mwenye miaka 11, walikuwa wameinama karibu na simu ya mkononi iliyotenganishwa sehemu zake, wakiainisha sehemu zake za ndani na kuelezea kazi zake husika.
Katika shule hiyo ya De'kayra, matarajio makubwa ya namna hiyo yanahimizwa tangu umri mdogo. Shule imejenga mbinu ya kufundisha inayochanganya kujifunza kitaaluma kwa kawaida na ukuzaji wa ujuzi wa vitendo, ikiakisi falsafa yake pana ya zaidi ya kujifunza kwa kufanya vitendo.
Kwa mujibu wa mwanzilishi na afisa mtendaji mkuu wa shule hiyo, Peter Peter Junior, wazo hilo lilianza zaidi ya miongo miwili iliyopita, kufuatia safari zake nje ya nchi, hasa China.
"Nilikwenda China mwaka 2005 kwa lengo la kutangaza mji wa kihistoria wa Bagamoyo kama kivutio cha watalii na kuvutia watalii zaidi wa China nilipokuwa nikifanya kazi katika utalii," amekumbushia.
"Kilichonivutia zaidi ilikuwa namna elimu ilivyochanganya nadharia na ujuzi wa vitendo. Maendeleo yao ya haraka ya kiteknolojia yanatokana na kujifunza kwa vitendo, mafunzo ya ufundi, na msisitizo mkubwa katika teknolojia ya kupashana habari na mawasiliano (TEHAMA)," Junior amesema.
Wakati wa kukaa nchini China, alitembelea shule za Shanghai na Hong Kong vilevile maeneo ya vijijini, akiona jinsi taasisi za kielimu zilivyorekebisha programu zao kulingana na mahitaji ya ndani na fursa za ajira za siku zijazo, kuanzia kilimo na ujenzi hadi teknolojia na uongozi.
Hali hiyo aliyojionea hatimaye ilichochea kuanzishwa kwa mfumo wa elimu wa De'kayra.
Hata hivyo, kwa Junior, lengo kuu linakwenda zaidi kujenga na kuzalisha wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani. Ni kuhusu kulea vijana ambao wanaweza kuchangia katika jamii, kutengeneza thamani, na kutafuta fursa kwa kujiamini.
"Tunawataka wawe washiriki wenye tija katika jamii," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




