

Lugha Nyingine
Wapalestina takriban 40 wauawa kwenye mashambulizi ya Israel katika mji wa Gaza (6)
![]() |
Ambulensi na watu wakionekana karibu na eneo la shambulizi la anga la Israel katika mji wa Gaza, Mei 7, 2025. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua) |
GAZA - Wapalestina takriban 40 wameuawa na makumi wengine kujeruhiwa kwenye mashambulizi ya Israeli katika mji wa Gaza jana Jumatano, kwa mujibu wa vyanzo vya afya vya Palestina ambapo mashuhuda wameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba droni ya Israel ilirusha angalau kombora moja kwenye mgahawa na soko katika kitongoji cha al-Rimal katikati mwa Gaza.
Vyanzo vya habari vya afya, vimeliambia Xinhua kwamba watu takriban 25 wameuawa kwenye shambulizi hilo la anga, huku makumi wengine wakijeruhiwa, wengi wao wakiwa katika hali mbaya.
Vyanzo hivyo vimeongeza kuwa watu waliojeruhiwa na miili ya waliofariki dunia wamepelekwa hospitalini, vikisema kuwa idadi ya vifo itaongezeka.
Wakati huo huo, mamlaka ya ulinzi wa raia ya Gaza imesema kuwa Wapalestina wasiopungua 15 wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika mashambulizi mawili ya anga ya Israel dhidi ya shule inayohifadhi watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa Mji wa Gaza.
Mahmoud Basal, msemaji wa mamlaka hiyo ya ulinzi wa raia, amesema Jeshi la Israel lililenga Shule ya Al-Karama, ambayo inahifadhi makumi ya familia zilizokimbia makazi kwenye kitongoji cha Al-Tuffah, katika mashambulizi mawili tofauti.
Basal amesema kuwa miongoni mwa waliofariki ni watoto na wanawake ambapo wote wamehamishiwa kwenye Hospitali ya Al-Ahli Arab katika Jiji la Gaza.
Ofisi ya vyombo vya habari vya serikali inayoongozwa na Hamas mjini Gaza imeripoti kwamba mwanahabari Nour al-Din Abdo ni miongoni mwa waliouawa, ikiongeza idadi ya waandishi waliouawa tangu Oktoba 7, 2023 hadi 213.
Katika taarifa yake, ofisi hiyo imelaani mauaji hayo yaliyofanywa na Jeshi la Israel dhidi ya waandishi wa habari wa Palestina na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa "kulaani uhalifu wa uvamizi huo ... na kufikisha wahalifu wa uvamizi huo mbele ya sheria."
Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka Jeshi la Israeli juu ya mashambulizi hayo ya anga.
Machi 18, Israeli ilirejea operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza. Wapalestina takriban 2,545 wameshauawa na wengine 6,856 kujeruhiwa tangu Israel iliporejea mashambulizi yake makali, ikiongeza jumla ya idadi ya vifo tangu Oktoba 2023 hadi 52,653, na majeruhi kufikia 118,897, mamlaka ya afya ya Gaza imesema jana Jumatano.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma