Mashambulizi ya droni yalenga maeneo ya kimkakati katika Mji wa Port Sudan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 07, 2025
Mashambulizi ya droni yalenga maeneo ya kimkakati katika Mji wa Port Sudan
Moshi ukifuka kwenda angani baada ya shambulizi la droni katika Mji wa Port Sudan, mashariki mwa Sudan, Mei 6, 2025. (Wizara ya Utamaduni na Habari ya Sudan/kupitia Xinhua)

KHARTOUM - Mashambulizi ya droni jana Jumanne yamepiga maeneo ya kimkakati katika Mji wa Port Sudan, mji wa bandari kwenye Bahari Nyekundu mashariki mwa Sudan, ikiwemo uwanja wa ndege wa kimataifa, hoteli moja iliyo karibu na ikulu ya muda ya rais, na bandari ya kusafirisha mafuta, kwa mujibu wa mashuhuda.

Ingawa hakuna kundi ambalo limedai kuhusika rasmi, jeshi la nchi hiyo limelaumu wanamgambo wa Vikosi vya Mwitikio wa Haraka (RSF) kwa mashambulizi hayo ya droni yaliyoanza Jumapili.

Shuhuda amesema mlipuko mkubwa katika ghala moja kusini mwa mji huo, wakati huohuo shahidi mwingine amesema droni imelenga Hoteli Marina karibu na majengo ya rais.

Afisa wa uwanja wa ndege, ambaye amekataa kutajwa jina, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba eneo la kiraia la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Port Sudan ulipigwa, ikilazimu kufutwa kwa safari zote za ndege zilizokuwa zimepangwa.

Wanaharakati wametoa picha za video zinazoonyesha moshi mwingi ukifuka kwenda angani juu ya Port Sudan, ambayo sasa imekuwa ikikabiliana na mashambulizi ya droni kwa siku tatu mfululizo.

Aidha, Kampuni ya Umeme ya Sudan imetangaza kuwa kituo cha transfoma cha Port Sudan pia kimelengwa kwa droni asubuhi ya leo (jana Jumanne), ikisababisha kukatika kabisa kwa umeme.

"Hii ni sehemu ya mashambulizi yanayolenga vituo vya umeme , ambayo inaathiri vibaya huduma za umma, zikiwemo huduma za maji na afya," kampuni hiyo imesema katika taarifa yake.

Serikali ya Sudan imelaani kile ilichokitaja kuwa "mashambulizi ya kigaidi ya droni."

"Nimemaliza punde kufanya ziara kwenye maghala ya mafuta katika bandari ya kusini ya Port Sudan, ambayo imekumbwa na mashambulizi ya kihalifu na kigaidi asubuhi ya leo (jana asubuhi) na droni zilizorushwa na wanamgambo wa Vikosi vya Mwitikio wa Haraka (RSF)," Khalid Ali Aleisir, msemaji wa serikali ya Sudan, amesema katika taarifa.

Msemaji huyo, ametoa hakikisho kuwa vikosi vya ulinzi wa raia na vyombo vya usalama vya nchi hiyo vinatekeleza wajibu wao kikamilifu na kusisitiza kuwa wananchi wa Sudan hawatatishwa na vitendo hivyo haramu.

RSF bado haijatoa maoni yoyote kuhusu mashambulizi hayo katika Mji wa Port Sudan.

Mei 4, RSF ilianzisha mashambulizi ya droni katika Mji huo wa Port Sudan kwa mara ya kwanza, yakilenga kambi ya jeshi la anga na miundombinu ya kiraia, wakati huohuo Mei 5, droni zilishambulia ghala la mafuta katika mji huo, na kuliharibu kabisa, kwa mujibu wa Wizara ya Nishati na Petroli ya Sudan.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha