Lugha Nyingine
'Kijiji T' cha Mkoa wa Guizhou, China: Kutoka milimani hadi jukwaa la kimataifa
Ndani ya bustani ya kitamaduni ya makabila huko Kaili, Eneo linalojiendesha la Makabila ya Wamiao na Wadong katika Mkoa wa Guizhou kusini-magharibi mwa China, onesho maalum la mitindo hufanyika kila jioni ya Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.
Wananaotembea kwenye jukwaa hilo la mitindo si wanamitindo wabobezi, bali ni wanakijiji wa kawaida kutoka wilaya jirani kama vile Rongjiang, Congjiang na Liping. Miongoni mwao kuna mafundi wa kudarizi na akina mama ambao hutumia siku zao kufanya kazi za kudarizi na kushona kwa mikono, kuendesha vibanda sokoni na kuhudumia familia zao.
Wakiwa wamevalia mavazi ya sherehe yariyodariziwa kwa rangi mbalimbali na kuwekwa mapambo ya silva, wanakijiji hao huonesha utamaduni wa kabila lao wanaoujivunia sana kwenye ufuatiliaji wa hadhira jukwaani.
Eneo hilo la Qiandongnan hapo awali lilikuwa moja ya maeneo makuu ya mapambano dhidi ya umaskini mkoani Guizhou. Siku za nyuma, milima ilikata usafiri na kufanya ujuzi mwingi uliorithiwa kutoka kizazi hadi kizazi kubaki ndani ya vijiji pekee.
Sanaa ya kudarizi, batiki na mapambo ya silva ya kabila la Wamiao ni zaidi ya kazi za mikono za kijadi. Kila vazi la kabila ni kama kitabu cha historia isiyoandikwa kinachovaliwa kwenye mwili, kikirekodi maisha ya vizazi vilivyopita na kubeba matumaini ya watu kwa maisha bora zaidi.
Julai 2024, kwa lengo la kuwapa wanakijiji fursa ya kuonesha mavazi yao ya sherehe, kijana wa kabila la Wamiao, Gu Axin, aliandaa onesho la mitindo la kijijini katika kijiji anakotokea. Kwa mshangao wake, watu wengi zaidi walijitokeza kushiriki, zaidi ya ambao wangeweza kuonesha mitindo yao katika siku moja au hata mbili.
"Kijiji T" kilianzishwa rasmi na hatua kwa hatua kikawa alama ya kung’ara ya utamaduni wa wenyeji. Hatimaye kilivuka mipaka ya vijiji na kufika kwenye majukwaa ya kimataifa, yakiwemo ya Wiki ya Mitindo ya China, Wiki ya Mitindo ya London, Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Wiki ya Mitindo ya New Zealand.
Zaidi ya jukwaa la mitindo, Soko la Urithi wa Utamaduni Usioshikika la Xiulitao limezipa sanaa hizi—ambazo hapo awali hazikupewa kipaumbele—nafasi katika soko pana zaidi. Vibanda zaidi ya 1,000 vimekusanyika hapa, na bidhaa za kudariziwa na za kazi za mikono zimefanikiwa kufika kwenye soko pana zaidi. "Kijiji T" kinaweka mkazo katika kuonesha na kutangaza utamaduni, wakati Soko la Xiulitao linatoa jukwaa kwa ajili ya ujasiriamali na biashara. Kwa pamoja, jukwaa hilo la maonesho ya mitindo na soko hilo vimeunganisha ufundi wa kijadi na maisha ya kisasa
Hadi kufikia mwaka 2026, "Kijiji T" cha Guizhou kimeshafanya maonesho zaidi ya 1,000, yakivutia washiriki zaidi ya 80,000 kutoka mamia ya vijiji vya jirani na kuonesha makumi ya maelfu ya mavazi ya makabila mbalimbali pamoja na kazi za urithi wa utamaduni usioshikika. Kimepokea watalii zaidi ya 900,000 na kufikia vijiji jirani zaidi ya 200.
"Kijiji T" pia kimeleta pamoja nyumba za wageni, migahawa, bidhaa za kitamaduni na ubunifu, na bidhaa maalum za kienyeji katika vijiji hivi, hali ambayo imetengeneza ajira zaidi ya 3,000. Kupitia mfumo wa "Kijiji T + Soko la Xiulitao," wastani wa kipato cha mwaka kwa wakazi wa vijiji hivyo kimeongezeka kwa yuan zaidi ya 12,000 kwa kila mtu, ongezeko la asilimia zaidi ya 40.
Leo hii katika eneo hilo la Qiandongnan, sindano na nyuzi za umri-wa kale bado zinadarizi ndege na vipepeo na kushona pamoja mtindo mpya wa maisha. Kama Rais wa China Xi Jinping—ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC)—alivyosisitiza katika ziara yake ya ukaguzi ya mkoani Guizhou, maeneo yenye idadi kubwa ya makabila madogo yanapaswa kuhifadhi tamaduni zao za kipekee na kuziachilia zing'ae kupitia maendeleo jumuishi ya utamaduni na utalii.
Kutoka milimani hadi jukwaa la kimataifa , simulizi ya "Kijiji T" ni kielelezo cha njia ya kipekee ya China katika kutokomeza umaskini. Wakati utamaduni uliorithiwa kutoka kwa vizazi vilivyopita unapogeuka kuwa tasnia mpya ya kiuchumi, na pale wakazi wa kawaida wa vijijini wanapokuwa chachu ya maendeleo, hata vijiji vilivyoko ndani kabisa ya milima vinaweza kufikia dunia pana zaidi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



