Lugha Nyingine
Saudi Arabia na Wahouthi warushiana vitisho huku mashambulizi dhidi ya vituo vya mafuta na miji yakizidi kupamba moto

Wafuasi wa kundi la Wahouthi wakishiriki katika maandamano ya silaha kupinga ushiriki wa Uturuki na Pakistan pamoja na Saudi Arabia kwenye mgogoro wa Yemen, jijini Sanaa, Yemen, tarehe 7 Oktoba 2026. (Picha na Mohammed Mohammed/Xinhua)
RIYADH/SANAA - Saudi Arabia na kundi la Wahouthi la Yemen zimerushiana vitisho vya mashambulizi ya kulipiza kisasi jana Jumanne huku mashambulizi ya kuvuka mpaka dhidi ya miji mikubwa na vituo vya mafuta yakiendelea.
Kwenye mkutano wa baraza la mawaziri jana Jumanne ulioongozwa na Mrithi wa Ufalme Mohammed bin Salman mjini Riyadh, Saudi Arabia imeonya kuwa Wahouthi wa Yemen watakabiliwa na madhara kutokana na mashambulizi yao ya mara kwa mara dhidi ya ufalme huo.
Baraza hilo la Mawaziri la Saudi Arabia limeusifu Muungano wa Kuunga Mkono Uhalali wa Serikali nchini Yemen kwa operesheni zake za kijeshi dhidi ya Wahouthi na kuahidi kulinda uhuru wa usafiri wa baharini katika Bahari Nyekundu na Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab.
Pia siku hiyo ya Jumanne, msemaji wa kijeshi wa Wahouthi, Yahya Sarea, alionya kuwa shambulizi lolote dhidi ya mji mkuu unaodhibitiwa na Wahouthi lingesababisha kile alichokitaja kuwa ni majibu "makali na yenye maumivu" dhidi ya Riyadh.
Baadaye kundi hilo lilionya kuhusu maeneo kadhaa nchini Saudi Arabia, vikiwemo vituo vinavyomilikiwa na kampuni kubwa ya mafuta ya Saudi, Aramco, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Khalid mjini Riyadh.
Mamlaka ya Ulinzi wa Raia ya Saudi Arabia imeitangaza mapema leo Jumatano kuwa watu wanne, wakiwemo wanawake wawili na mtoto mmoja, wamejeruhiwa na nyumba 15 za makazi zimeharibiwa baada ya vipande vya makombora mawili ya 'cruise' yaliyozuiwa kuangukia mji mkuu, Riyadh jana Jumanne.
Wakati huo huo, jengo la utawala la Saudi Aramco mjini Dhahran, katika Jimbo la Mashariki la Saudi Arabia, lililengwa jioni jana Jumanne na kusababisha moto kiasi, Shirika la Habari la Saudi limeripoti mapema leo Jumatano.
Usiku wa jana Jumanne, muungano huo ulisema kuwa ulizuia makombora na droni kadhaa juu ya maeneo ya mashariki na kusini mwa Saudi Arabia. Pia umeripoti kuzuia kombora la 'balestiki' lililokuwa likilenga kituo cha utawala katika Mkoa wa Al-Ahsa katika Jimbo la Mashariki.
Wahouthi walisema jana Jumanne kuwa ndege za kivita na makombora ya Saudi Arabia yalifanya mashambulizi 104 katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.
Msemaji wa Wahouthi amedai kuwa mashambulizi hayo yamesababisha vifo na majeraha kwa raia, bila kutoa takwimu mahususi. Mjini Sanaa, mashambulizi yalilenga Kituo Kikuu cha Al-Sabaha cha Kampuni ya Mafuta ya Yemen, ambacho ni kituo cha kuhifadhi na kusambaza mafuta kilicho magharibi mwa jiji hilo.
Huku hayo yakiendelea, juhudi za kidiplomasia zimeshika kasi. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, katika mazungumzo ya simu jana Jumanne, alimwambia mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, kuwa Uturuki inaunga mkono kwa dhati Saudi Arabia na itaendelea kusimama pamoja na Riyadh.
Pia katika siku hiyo ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Prince Faisal bin Farhan bin Abdullah, alifanya mazungumzo ya simu kwa nyakati tofauti na wenzake wa Qatar, Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambao walilaani mashambulizi hayo ya Wahouthi na kusisitiza tena mshikamano wao na ufalme huo.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alijadili suala la kupunguza kupamba moto kwa mvutano katika eneo hilo na wenzake wa Uturuki, Iraq na Misri, akisisitiza umuhimu wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo. Juzi Jumatatu, Tehran ilisisitiza tena utayari wake wa kusaidia kuwezesha mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Wahouthi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



