Lugha Nyingine
Benki ya Stanbic Tanzania yazindua huduma ya malipo ya moja kwa moja kwa RMB ili kuwezesha biashara na China
Benki ya Stanbic Tanzania, moja ya benki zinazoongoza za kibiashara nchini Tanzania, Jumatano ilizindua huduma ya malipo ya moja kwa moja kwa Renminbi (RMB), ikiruhusu wafanyabiashara wa Tanzania wanaofanya biashara na China kutoa na kupokea malipo moja kwa moja kwa sarafu ya China, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za miamala na kuwezesha biashara ya pande mbili.
Akibainisha kuwa uzinduzi huo unatengeneza fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki kwa ufanisi zaidi katika masoko ya kimataifa, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania Dennis Londo amesema mauzo ya nje ya Tanzania kwenda China yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 442.96 mwaka 2024 hadi dola milioni 512.6 mwaka 2025, huku uagizaji ukiongezeka kutoka dola bilioni 4.78 hadi dola bilioni 5.64.
Londo amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa China kuwa mshirika wa biashara, na malipo hayo ya moja kwa moja kwa RMB yanaweza kupunguza hatua zisizo za lazima za ubadilishaji wa fedha kwa waagizaji wa Tanzania na kuwapa wauzaji bidhaa nje utaratibu wa ziada wa kupokea malipo kutoka kwa wanunuzi wa China.
Naye Balozi wa Tanzania nchini China Suleiman Haji Suleiman ameihimiza Benki ya Stanbic Tanzania kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wafanyabiashara walio zaidi ya vituo vikubwa vya kibiashara na kutoa mwongozo wa kivitendo kuhusu miamala ya RMB, usimamizi wa kubadilisha fedha za kigeni, mambo ya nyaraka na ufuataji wa sheria.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



