Lugha Nyingine
Iran yasema ada za huduma zinapaswa kutozwa kwa upitaji kwenye Mlango Bahari wa Hormuz

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei akizungumza kwenye mkutano wa wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Agosti 10, 2026. (Xinhua/Shadati)
TEHRAN - Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema ada zinapaswa kutozwa kwa huduma za baharini zinazotolewa kwenye Mlango Bahari wa Hormuz.
Ametoa kauli hiyo jana Jumatatu kwenye mkutano wa wiki na waandishi wa habari wakati akijibu swali kuhusu kama ada za huduma za baharini zimejadiliwa kwenye mazungumzo kati ya Iran na Oman kuhusu upangaji njia mpya kwenye mlango bahari huo wa maji.
"Kwa ujumla, unapotoa huduma za baharini, lazima urudishiwe malipo kwa ajili yake," Baghaei amesema.
"Katika hatua hii, hatujadili vipengele kama hivyo," amesema, akiongeza kuwa majadiliano yanaendelea na "pointi fulani za kiufundi" zitajadiliwa.
Baghaei amesema mazungumzo kati ya Iran na Oman "yanafanyika vizuri na kiujenzi," akibainisha kuwa mifumo itaanzishwa ili kuhakikisha usafirishaji salama, kushughulikia masuala ya mazingira, kutoa huduma za baharini na kupambana na uhalifu kwenye mlango bahari huo.
"Chini ya makubaliano yanayoweza kufikiwa kati ya pande hizo mbili, njia ya kati itakuwa mbadala wa njia zilizopo sasa za kaskazini na kusini kwenye mlango bahari," amesema, akiongeza kuwa njia hiyo mpya itatumika kwa muda hadi pale Iran na Oman zitakapokubaliana kuhusu mpango mpya wa kutenganisha upitaji wa meli.
Baghaei amehusisha kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz na "uchokozi wa kijeshi" wa Marekani na Israeli dhidi ya Iran, akisema kufunguliwa kwake kunategemea kuondolewa kwa masharti yaliyowekwa kwa Iran.
Amerudia kwamba Iran haifanyi mazungumzo na Marekani, lakini nchi hizo mbili zinaendelea kutumiana ujumbe mbalimbali kupitia wapatanishi.
Iran iliimarisha nguvu zake za umiliki kwenye Mlango Bahari wa Hormuz Februari 28 kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israeli katika eneo la Iran.
Juni 18, Iran na Marekani zilisaini nyaraka ya makubaliano juu ya kumaliza vita. Chini ya makubaliano hayo, nchi hizo mbili zilikuwa zimepangwa kufanya mazungumzo ndani ya siku 60 ili kufikia makubaliano ya mwisho, lakini mustakabali wa mazungumzo hayo umekuwa si wa uhakika kufuatia kupamba moto kwa mivutano kati ya pande hizo mbili mwezi uliopita .
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



