Wapalestina waliokimbia makazi waanza kurudi Kaskazini mwa Gaza wakati makubaliano ya kusimamisha mapigano yakianza kutekelezwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 11, 2025

GAZA/JERUSALEM - Wapalestina waliokimbia makazi yao wameanza kurudi kutoka sehemu ya kusini mwa Ukanda wa Gaza kuelekea kaskazini baada ya Jeshi la Israel kutangaza kuwa raia wanaruhusiwa kupita katika barabara ya Rashid na Salah al-Din ya pwani, vyanzo vya habari mjini Gaza vimesema jana Ijumaa.

Mjongeo huo wa raia umekuja muda mfupi baada ya makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya Israeli na Hamas kuanza kutekelezwa rasmi jana mchana kwa saa za Mashariki ya Kati, yakihitimisha miaka miwili ya vita ambavyo vimeacha makumi kwa maelfu ya watu wakiwa wameuawa na kusababisha uharibifu mkubwa katika ukanda huo.

Katika taarifa yake, Jeshi la Ulinzi la Israel limesema vikosi vyake vimepangwa kwenye safu mpya kulingana na masharti ya makubaliano na mfumokazi wa kurudisha mateka. Limeongeza kuwa wanajeshi walio chini ya Kamandi ya Kusini wataendelea kufuatilia hali ya mambo na kujibu vitisho vyovyote vya mara moja kwa usalama wa Israel.

Kwenye ujumbe wake kwa wakazi wa Gaza, msemaji wa jeshi hilo Avichay Adraee amesema wanajeshi wa Israel wataendelea kuwepo katika maeneo maalum ndani ya Ukanda wa Gaza na kuonya raia dhidi ya kukaribia maeneo ya kijeshi "hadi taarifa zaidi itakapotolewa."

Ametahadharisha raia kuepuka Beit Hanoun, Beit Lahia, na al-Shuja'iyya katika sehemu ya kaskazini, vilevile Rafah na Ushoroba wa Philadelphi katika upande wa kusini, akiyaelezea kuwa maeneo yaliyo hatarini.

Adraee pia amehimiza wakaazi kuwa mbali na maeneo ya bahari na mpakani, akiwashauri dhidi ya uvuvi au kuogelea katika siku zijazo.

Vyanzo vya habari vya usalama na mashuhuda katika Ukanda wa Gaza wameripoti kwamba milio ya makombora na risasi ilikoma kabisa katika Ukanda wa Gaza wakati usimamishaji mapigano ulipoanza rasmi na kwamba utulivu wa tahadhari ulikuwa umetawala katika Mji wa Gaza, eneo la kati, Khan Younis na Rafah kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi kadhaa.

Maelfu ya Wapalestina waliokimbia makazi yao walionekana wakitembea au kuendesha magari kuelekea kaskazini kwenye Barabara ya Rashid ya pwani, ambayo imefunguliwa tena kwa matumizi kufuatia kuondolewa kwa magari ya kijeshi ya Israeli kutoka eneo hilo.

Mjongeo wa watu wengi pia umeripotiwa katika Barabara ya Salah al-Din huku familia zaidi zikianza kurudi kwenye makazi yao kaskazini mwa Gaza.

"Tunarudi licha ya uharibifu; jambo la muhimu zaidi ni kwamba vita vimekoma na watoto wetu wako salama," Mohammed al-Louh, mkaazi aliyekimbia kutoka Mji wa Gaza, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Ameuelezea wakati huo kuwa ni "mwanzo wa kurudi kwa maisha baada ya miaka miwili ya shida."

Miaka miwili ya mashambulizi ya Israel yameiacha Gaza ikiwa katika magofu, yakisababisha njaa, na kuua watu zaidi ya 67,000, kwa mujibu wa mamlaka za afya za Gaza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha