Israel na Hamas zajiandaa kutekeleza makubaliano ya kusimamisha mapigano Gaza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 10, 2025

GAZA/JERUSALEM - Israel na Hamas zinajiandaa kutekeleza makubaliano ya kusimamisha mapigano Gaza, huku hafla rasmi ya kutia saini ikiwa imefanyika jana Alhamisi mjini Sharm el-Sheikh, Misri kufuatia siku tatu za mazungumzo makali yaliyopatanishwa na Misri, Qatar, Uturuki na Marekani, vyanzo vya habari ndani ya Palestina na Israel vimesema.

Afisa mwandamizi wa Hamas Osama Hamdan ameuambia Mtandao wa Televisheni ya Alaraby ya Qatar katika mahojiano jana Alhamisi kwamba usimamishaji huo mapigano utaanza mara moja baada ya idhini ya serikali ya Israel.

"Awamu ya kwanza ya makubaliano inajumuisha kujiondoa kwa Israel kutoka Mji wa Gaza, kaskazini, Rafah, na Khan Younis, na kufunguliwa kwa vivuko vitano kwa ajili ya kuingia kwa misaada ya kibinadamu, huku mashirika ya kimataifa yakisimamia usambazaji misaada," amesema.

Ameongeza kuwa operesheni za droni katika anga ya Ukanda wa Gaza zitakoma wakati wa mchakato wa kuachilia huru wafungwa, ambao utahusisha wafungwa 250 wa Kipalestina wanaotumikia vifungo vya maisha na wafungwa wengine 1,700.

Chanzo cha habari kilicho karibu na Hamas, kikizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, kimeliambia Shirika la Habari la China, Xinhua siku hiyo ya Alhamisi kwamba kundi hilo limeanza kuhamisha mateka wa Israel na kuwapeleka katika maeneo salama ndani ya Ukanda wa Gaza kwa ajili ya maandalizi ya kuwakabidhi kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu katika siku zijazo.

Wakati huhuo Serikali ya Israel mapema leo Ijumaa imeidhinisha makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano na Hamas ili kumaliza vita mjini Gaza na kuhakikisha kuachiliwa huru kwa mateka wote waliosalia.

Chini ya masharti ya makubaliano hayo, ambayo nakala yake Shirika la Habari la China, Xinhua limeweza kuipata, usimamishaji huo mapigano sasa umeanza rasmi.

"Serikali sasa imeidhinisha mfumokazi wa kuachiliwa huru kwa mateka wote -- walio hai na waliofariki," ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema katika taarifa.

Mpango huo umepata kura za kutosha, ingawa mawaziri wanaounga mkono walowezi Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich, miongoni mwa wengine, wamepiga kura ya kuupinga.

Mapema siku hiyo ya Alhamisi, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba Israel na Hamas zimekubaliana na "awamu ya kwanza" ya mpango wake wa pointi 20 wa kumaliza mgogoro huo wa miaka miwili mjini Gaza, na kuachiliwa huru mateka wa Israel na baadhi ya wafungwa wa Kipalestina. Habari zinaeleza kuwa Trump anaweza kuzuru Israel siku ya Jumapili ili kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha