

Lugha Nyingine
UN iko tayari kuongeza misaada ya kibinadamu kwa Watu wa Gaza kufuatia makubaliano ya kusimamisha mapigano: Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Oktoba 9, 2025. (Xinhua/Xie E)
UMOJA WA MATAIFA - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema jana Alhamisi kuwa chombo hicho cha dunia kiko tayari kuongeza misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza kufuatia tangazo la makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya Israel na Hamas.
"Umoja wa Mataifa utatoa uungaji wake mkono kamili. Sisi na washirika wetu tumejitayarisha kwenda -- sasa. Tuna utaalamu, mitandao ya usambazaji, na uhusiano wa jamii vilivyoko tayari kuchukua hatua. Vitu vipo, na timu zetu ziko katika hali ya kusubiri. Tunaweza kuongeza msaada wa chakula, maji, matibabu na malazi mara moja." Guterres amewaambia waandishi wa habari.
Amesisitiza kuwa kunyamazisha bunduki hakutoshi kugeuza usimamishaji huo mapigano kuwa upigaji hatua halisi.
"Tunahitaji ufikaji kamili, salama na endelevu wa wafanyakazi wa kibinadamu; kuondolewa kwa urasimu na vizuizi; na kujengwa upya kwa miundombinu iliyobomolewa. Na tunahitaji Nchi Wanachama (wa UN) kuhakikisha kuwa shughuli za kibinadamu zinafadhiliwa ipasavyo ili kukidhi mahitaji makubwa," amesema.
Amesema, kwa Waisraeli na Wapalestina sawia, makubaliano hayo yanatoa mwanga wa ahueni. Mwanga huo lazima uwe mwanzo wa amani, na kuanza kwa mwisho wa vita hivyo vya uharibifu.
"Ninahimiza wote kutumia kikamilifu fursa hii muhimu kuanzisha njia ya kisiasa inayoaminika kusonga mbele. Njia ya kuelekea kukomesha ukaliaji huo kwa mabavu, kutambua haki ya kujitawala kwa watu wa Palestina, na kufikia suluhisho la nchi mbili. Njia ya kuelekea amani ya haki na ya kudumu kati ya Waisraeli na Wapalestina -- na kwa amani na usalama zaidi katika Mashariki ya Kati," amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.
Amebainisha kuwa mafanikio haya yanadhihirisha nguvu na uwezo bora wa diplomasia na ni ukumbusho kuwa masuluhisho ya migogoro hayapatikani kwenye medani ya vita. "Lazima yapatikane kwenye meza ya mazungumzo, na kisha, muhimu zaidi, lazima zitekelezwe kikamilifu," Guterres amesema.
Amekaribisha tangazo hilo la Jumatano la makubaliano ya kufikia usimamishaji mapigano mjini Gaza na kuachiliwa huru kwa mateka, kulingana na pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump. Pia amepongeza juhudi za kidiplomasia za Marekani, Qatar, Misri na Türkiye katika kufanikisha mafanikio hayo.
Guterres amehimiza pande zote kutii kikamilifu masharti ya makubaliano hayo na kukumbatia kikamilifu fursa zinazotolewa nayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Oktoba 9, 2025. (Xinhua/Xie E)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Oktoba 9, 2025. (Xinhua/Xie E)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma