

Lugha Nyingine
Biashara ya nje ya China yadumisha ukuaji tulivu licha ya changamoto kali kutoka nje
Picha hii inaonyesha magari yanayosubiri kusafirishwa kuuzwa nje kwenye Bandari ya Yantai, Mkoa wa Shandong, mashariki mwa China, Januari 2, 2025. (Picha na Tang Ke/Xinhua)
BEIJING - Thamani ya jumla ya biashara ya uagizaji na uuzaji nje bidhaa ya China kwa kipimo cha yuan iliongezeka kwa asilimia 3.5 mwezi Agosti kuliko mwaka jana wakati kama huo, ikimaanisha mwezi wa tatu mfululizo ambapo zote biashara za uagizaji na uuzaji nje bidhaa zimepata ukuaji sambamba, takwimu rasmi kutoka Mamlaka Kuu ya Forodha ya China (GAC) zimeonyesha jana Jumatatu.
Kwa mujibu wa GAC, katika kipindi cha Januari hadi Agosti, biashara ya uagizaji na uuzaji nje bidhaa ya China pia iliongezeka kwa asilimia 3.5.
"Mauzo ya nje yaliongoza upanuzi wa jumla katika kipindi cha Januari hadi Agosti, yakiongezeka kwa asilimia 6.9 kuliko mwaka jana wakati kama huo, huku uagizaji bidhaa kutoka nje ulirekodi punguo dogo kwa asilimia 1.2" GAC imesema.
Mamlaka hiyo imesema kuwa, kwa kipimo cha dola za Marekani, thamani ya biashara hiyo ya uagizaji na uuzaji nje bidhaa ya nchi hiyo ilifikia dola za Marekani bilioni 321.81 na dola za Marekani bilioni 219.48, mtawalia, mwezi Agosti.
Imesema kuwa, kwa muda wa miezi minane ya kwanza, takwimu hizo zilikuwa dola za kimarekani trilioni 2.452 na trilioni 1.666, mtawalia.
Katika kipindi cha Januari hadi Agosti, ASEAN ilibaki kuwa mwenzi mkubwa zaidi wa kibiashara wa China, huku jumla ya biashara ya pande mbili ikiongezeka kwa asilimia 9.7 hadi kufikia yuan trilioni 4.93 (dola za Kimarekani karibu bilioni 686.8), ikichukua asilimia 16.7 ya jumla ya biashara ya nje ya nchi hiyo. Imefuatiwa na Umoja wa Ulaya, ambapo biashara kati yake na China iliipanda kwa asilimia 4.3, takwimu hizo zinaonyesha.
China imeendelea kuwa mwenzi mkubwa zaidi wa kibiashara wa ASEAN kwa miaka 16 mfululizo, wakati huohuo ASEAN imekuwa mwenzi mkuu wa kibiashara wa China kwa miaka mitano mfululizo.
Takwimu hizo pia zinaonyesha ongezeko la asilimia 5.4 katika biashara na nchi za Ukanda Mmoja, Njia Moja hadi kufikia yuan trilioni 15.3, wakati biashara na Marekani, mwenzi wa tatu wa kibiashara wa China, ilishuka kwa asilimia 13.5 katika miezi minane ya kwanza ya mwaka huu.
Ufanisi huo wa biashara umekuja huku kukiwa na hali ya kutokuwa na uhakika katika maendeleo ya uchumi na biashara duniani, huku mashirika kadhaa ya kimataifa yakisema kuwa vizuizi vya ushuru vimeongeza kwa kiasi kikubwa gharama za biashara ya kimataifa.
Wizara ya biashara ya China imeahidi kupanua ufunguaji mlango wa kiwango cha juu, huku nchi hiyo ambayo ni mfanyabiashara mkubwa zaidi wa bidhaa duniani ikishughulikia hali hiyo ya kutokuwa na uhakika kwa maendeleo bora ya hali ya juu.
Lyu Daliang, mkurugenzi wa Idara ya Takwimu na Uchambuzi wa GAC, amesema kuwa biashara ya bidhaa ya China imedumisha mwelekeo wake wa ukuaji tulivu licha ya kukabiliwa na mazingira magumu na yenye changamoto ya nje.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma