China yatoa wito wa kufikiwa kwa usimamishaji vita wa kweli katika Mashariki ya Kati

(CRI Online) Juni 25, 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Wang Yi amesema, China inaunga mkono juhudi za Iran za kulinda mamlaka na usalama wa taifa, na kwa msingi huo, kufikia usimamishaji vita wa kweli, kurejesha maisha ya kawaida ya watu, na kusaidia kupunguza hali ya mvutano katika Mashariki ya Kati haraka iwezekanavyo.

Wang, ametoa kauli hiyo kwenye mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Iran Bw. Seyed Abbas Aragchi jana Jumanne, akieleza kuwa China inatumai Iran itaendelea kuhakikisha usalama wa taasisi, wafanyakazi na wanadiplomasia wa China nchini humo.

Kwa upande wake, Bw. Aragchi amesisitiza kuwa, hatua za hatari za Israel na Marekani katika kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, ikiifanya Iran kutokuwa na uamuzi mwingine zaidi ya kujibu.

Amesema mazungumzo ya kweli yanaweza tu kuanza mara tu Israel itakapositisha uchokozi wake, na kuongeza kuwa Iran inapenda kudumisha mawasiliano ya karibu na China na kwamba inatarajia mchango mkubwa wa China katika kupunguza mvutano huo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha