WFP yapunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi zaidi ya milioni moja nchini Uganda kutokana na ukosefu wa fedha

(CRI Online) Mei 08, 2025

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limepunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi milioni moja nchini Uganda kutokana na ukosefu wa fedha.

Shirika hilo Jumanne lilitoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii likisema, linahitaji sana dola milioni 50 za kimarekani ili kurejesha misaada ya kuokoa maisha ya wakimbizi na wale wanaotafuta hifadhi nchini Uganda.

WFP imeonya kuwa kiwango cha utapiamlo katika vituo vya kupokea wakimbizi kimezidi asilimia 15, ikisisitiza kuwa inahitaji fedha za dharura kuokoa maisha ya watu hao.

Mwezi Machi, WFP ilitangaza kupunguza mgao wa chakula kwa familia za wakimbizi nchini Uganda, ambapo wakimbizi wapya walipata asilimia 60 tu ya chakula cha msaada badala ya asilimia 100, walio katika mazingira magumu zaidi walipata asilimia 40, chini kutoka asilimia 60, na kaya zilizo katika mazingira magumu kiasi zimeshuhudia mgao wao ukipungua kutoka asilimia 30 hadi asilimia 22.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha