Azma ya China ya kulinda maslahi yake ya maendeleo haitabadilika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 08, 2025

Mazungumzo ya ngazi ya juu ya uchumi na biashara kati ya China na Marekani yatafanyika nchini Uswisi hivi karibuni. Mkutano huo unafanyika kwa ombi la Marekani. Msimamo wa China ni thabiti. Iwe kupigana au kuzungumza, azma ya China ya kulinda maslahi yake ya maendeleo haitabadilika, na msimamo na lengo lake la kutetea haki na usawa wa kimataifa na kudumisha utaratibu wa kimataifa wa uchumi na biashara hautabadilika.

Hivi karibuni, maafisa waandamizi wa Marekani wamekuwa wakivujisha kila mara habari kuhusu kurekebisha hatua za kodi na kwa bidii kufikisha taarifa kwa China kupitia njia mbalimbali, wakitumai kuzungumza na China kuhusu kodi na masuala mengine. Kwa misingi ya kuzingatia kikamilifu matarajio ya kimataifa, maslahi ya China, na miito ya viwanda na wanunuzi wa Marekani, China imeamua kukubali kuzungumza na Marekani, jambo ambalo linaonyesha mtazamo wa China wa kuwajibika. Kama Marekani kwa dhati inatumai kutatua suala hilo kwa njia ya mazungumzo na majadiliano, inapaswa, kwa moyo wa "kushika neno lake na kutenda ipasavyo", kubadili kauli yake kuwa marekebisho madhubuti ya sera na kushiriki katika mashauriano na mazungumzo ya kitaalamu na kivitendo na China.

Kiasi cha jumla cha uchumi wa China na Marekani kinazidi 1/3 ya dunia, jumla ya watu wa nchi hizo wanachukua karibu 1/4 ya dunia, na kiasi cha biashara ya pande mbili kinachukua takriban 1/5 ya dunia. Kiini cha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani ni kunufaishana na manufaa ya pande zote. Msururu wa hatua haramu na zisizo na sababu za kutoza kodi ya upande mmoja zilizochukuliwa na serikali mpya ya Marekani zimeathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani, kuvuruga kwa sehemu kubwa utaratibu wa kimataifa wa uchumi na biashara, na pia kuleta changamoto kubwa katika kuimarika na kukua kwa uchumi wa dunia. Ili kutetea haki na maslahi yake halali na haki na usawa wa kimataifa, China imechukua hatua madhubuti na za nguvu dhidi ya matumizi mabaya ya kodi ya Marekani. Matumizi hayo mabaya ya kodi ya Marekani pia yameharibu vibaya maslahi ya kampuni na wanunuzi wa Marekani, na madhara yake yanajitokeza.

Marekani imefanya hesabu isiyo sahihi kwa kutumia vibaya kodi kwa China na kutoa shinikizo la juu kwa upofu. Mafanikio ya maendeleo ya China ni matokeo ya kazi ngumu ya watu wa China, si matokeo ya neema ya yeyote. China ina imani kubwa ya "kupigana hadi mwisho". Haijalishi namna gani hali ya kimataifa hubadilika, China itajikita katika kufanya mambo yake yenyewe, siku zote itapanua ufunguaji mlango bila kuyumbayumba, kudumisha bila kuyumba mfumo wa biashara wa pande nyingi huku WTO ikiwa msingi wake, na kugawana bila kuyumba fursa za maendeleo na nchi mbalimbali duniani.

Maendeleo yenye afya ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani yanahitaji pande zote mbili kusongeshana mbele. China muda wote imekuwa ikiamini kwamba mazungumzo na majadiliano yoyote lazima yafanywe kwa msingi wa kuheshimiana, mashauriano ya usawa na kunufaishana. Kama Marekani itasema jambo moja na kufanya lingine, au hata kujaribu kuendelea kutumia mabavu na ulaghai chini ya kivuli cha mazungumzo, China haitakubali kamwe.

Historia na uhalisia vimethibitisha mara kwa mara kwamba China na Marekani zitafaidika kutokana na ushirikiano na kupoteza kutoka kwenye makabiliano. Marekani inapaswa, kwa msingi wa kanuni za kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote, kutatua mambo yao husika kupitia mazungumzo na mashauriano yenye usawa na China, kwa pamoja kuhimiza maendeleo yenye afya, tulivu na endelevu ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani, na kuweka uhakika zaidi katika uchumi wa dunia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha