

Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa Canada asema mazungumzo na Trump ni ya kiujenzi licha ya kutoondolewa kwa ushuru
Rais wa Marekani Donald Trump (katikati) akimkaribisha Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney (kulia) katika Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Mei 6, 2025. U.S. (Xinhua/Hu Yousong)
OTTAWA - Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney amesema alifanya mazungumzo mapana na ya kiujenzi na Rais wa Marekani Donald Trump Jumanne katika Ikulu ya White House, ingawa viongozi hao wawili hawakukubaliana juu ya kuondoa ushuru na "Jimbo la 51," kwa mujibu wa matangazo ya moja kwa moja ya Shirika la habari la CBC.
Akifanya mkutano na wanahabari baada ya mkutano huo mjini Washington, D.C., Carney amesema kwamba yeye na Trump wamekubaliana kuwa na mazungumzo zaidi katika wiki zijazo na kukutana tena ana kwa ana kwenye mkutano wa kilele wa G7 mjini Kananaskis, Alberta.
Carney amesema amemwambia Trump "haina maana" kurudia wazo la Jimbo la 51, akiongeza kuwa Trump ni rais ambaye atasema chochote anachotaka. "Anaelewa kuwa tuna mazungumzo kati ya mataifa huru," Carney amesema.
Akijibu swali kama anarejea Ottawa na maendeleo halisi katika kumaliza vita vya biashara, Carney amesema walikuwa na mambo maalum ya kufuatilia na kujenga kwayo kutoka hapo.
"Hii ni mijadala mnayofanya wakati mnatafuta suluhu," amesema.
Wakati Trump ameweka wazi kwamba ushuru, haswa uliowekwa kwenye sekta ya magari, utabaki mahali pake, Carney amesema, "Tutaona."
Wafanyakazi na wauzaji bidhaa wa Canada katika miji ya viwanda vya magari wana wasiwasi kwamba kadiri mzozo wa ushuru unavyoendelea, ndivyo uwezekano mdogo wa magari yaliyomalizika kuuzwa, CBC imeripoti.
Trump awali alichapisha taarifa kwenye akaunti yake ya Mtandao wa Truth Social dakika chache kabla ya kuwasili kwa Carney katika Ikulu ya White House, akidharau umuhimu wa Canada kwa uchumi wa Marekani.
"Hatuhitaji Magari yao, hatuhitaji Nishati yao, hatuhitaji Mbao zao, hatuhitaji kitu chochote walichonacho. Wao, kwa upande mwingine, wanahitaji KILA KITU kutoka kwetu!" aliandika Trump.
Akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi ya Oval mapema Jumanne, Trump alisema Makubaliano kati ya Marekani na Mexico-Canada (USMCA) ni "hatua ya mpito" ambayo "itakoma kwa muda mfupi," bila kutoa maelezo yoyote juu ya kuhuishwa kwake.
Trump amerudia vitisho vya unyakuaji eneo dhidi ya Canada, ambayo amesema itakuwa "ndoa nzuri" na kuuita tena mpaka kati ya nchi hizo mbili "usio halisi".
Rais huyo amesema itakuwa bora kwa Canada kuwa "jimbo la 51" la Marekani huku likiwa na faida nyingi, kupunguzwa kwa ushuru na jeshi huru.
Wakati Carney aliingilia na kusema kwamba Canada "kamwe si kwa ajili ya kuuzwa," Trump alitania, "Kamwe usiseme kamwe, ... muda utaongea."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma