

Lugha Nyingine
Naibu waziri mkuu wa China ataka kufanya juhudi zote za matibabu baada ya ajali ya boti mkoani Guizhou, China
Naibu Waziri Mkuu wa China Zhang Guoqing, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akisikiliza kuhusu shughuli za utafutaji na uokoaji kwenye eneo la tukio baada ya ajali ya boti kupinduka katika Mji wa Qianxi wa Bijie, Mkoa wa Guizhou, kusini-magharibi mwa China, Mei 5, 2025. (Xinhua/Yan Yan)
GUIYANG – Naibu Waziri Mkuu wa China Zhang Guoqing amehimiza juhudi zote za uokoaji na matibabu kufuatia ajali ya kupinduka kwa boti kadhaa katika Mkoa wa Guizhou kusini magharibi mwa China.
Upepo mkali wa ghafla juzi Jumapili alasiri ulisababisha boti nne kupinduka katika mto wa Mji wa Qianxi mkoani humo, na watu 84 kuanguka maji. Wote waliohusika katika ajali hiyo walikuwa wamepatikana hadi kufikia saa 6:45 mchana, jana Jumatatu, huku 10 wakiwa wamefariki, 70 kujeruhiwa na wanne bila kujeruhiwa.
Zhang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), alikwenda kwenye eneo la ajali na baadaye hospitali ya eneo hilo ili kuongoza juhudi za uokoaji na matibabu.
Wataalam wa matibabu na rasilimali zinapaswa kuhamasishwa kikamilifu kutibu majeruhi ili kupunguza vifo na ulemavu, amesema kwenye mkutano mapema Jumatatu asubuhi, akihimiza kufanya juhudi zote za uungaji mkono kwa familia zinazofiwa.
Kuhusu hatua za usalama, ametoa wito wa kuimarishwa kwa viwango vya usimamizi wa usalama, vikiwemo vile vinavyohusu kuzuia ajali, kutambua hatari na kurekebisha masuala, kwa lengo la kuzuia na kudhibiti ipasavyo matukio makubwa ya usalama katika siku zijazo.
“Msisitizo unapaswa kuelekezwa katika maeneo muhimu kama vile vivutio vya utalii, maeneo makubwa ya umma, jumuiya za makazi na sekta za usafirishaji ili kutambua na kuondoa hatari,” amesema.
Zhang amesema, ufuatiliaji hali ya hewa kali na mifumo ya tahadhari ya mapema vinapaswa kuimarishwa, kwa mwitikio dhahiri na michakato ya uratibu wa dharura, wakati huohuo hatua za kuzuia ufikiaji wa maeneo ya utalii na kupunguza uendeshaji wa meli za abiria wakati wa hali mbaya ya hewa lazima zitekelezwe ili kuhakikisha usalama wa umma.
Naibu Waziri Mkuu wa China Zhang Guoqing, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akimtembelea mtu aliyejeruhiwa kwenye ajali ya boti kupinduka hospitalini katika Mji wa Qianxi wa Bijie, Mkoa wa Guizhou, kusini-magharibi mwa China, Mei 5, 2025. (Xinhua/Yan Yan)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma