

Lugha Nyingine
China yalaani “kutozana kodi kwa usawa” wa Marekani kwenye mkutano wa WTO
GENEVA – China imekanusha shutuma za “uwezo wa uzalishaji kupita mahitaji ya soko” zilizotolewa na Marekani na baadhi ya nchi zingine kwenye mkutano wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), na imelaani “kutozana kodi kwa usawa” na sera za ruzuku ya kubagua za Marekani kwa kupuuza kwa kiwango kikubwa kanuni za WTO.
Akizungumza kwenye mkutano wa Jumanne wa Kamati ya Ruzuku na Hatua za Kuzuia Utoaji Ruzuku, ujumbe wa China umesisitiza kuwa hakuna kiwango au mbinu inayotambulika duniani kuelezea uwezo wa uzalishaji kupita mahitaji ya soko.
Ujumbe huo umeeleza kuwa uzalishaji wa nchi mwanachama wa WTO hauwezi tu kukidhi mahitaji yake ya ndani bali pia ni kwa ajili ya kuiwezesha kushiriki katika biashara ya kimataifa na ushindani wa soko kwa misingi ya faida linganishi za ushindani alizonazo.
“Kwa mfano, Marekani husafirisha kuuza nje kiasi kikubwa cha chipu za semiconductor, ndege na maharage ya soya, wakati Ujerumani na Japan ni wauzaji wakubwa wa magari nje ya nchi” umeeleza ujumbe huo.
Simulizi ya “uwezo wa uzalishaji kupita mahitaji ya soko” inayovumishwa na Marekani na baadhi ya nchi zingine wanachama inapingana na mantiki ya utandawazi wa kiuchumi, na badala yake inaonyesha hofu kuhusu ushindani na sehemu ya soko, ujumbe huo wa China umesema, ukiongeza kuwa “uzalishaji kupita mahitaji ya soko” ni kisingizio dhaifu kuhalalisha hatua za upande mmoja na za kujihami.
Ujumbe huo umesisitiza kuwa maendeleo ya viwanda ya China na faida zake za ushindani si matokeo ya ruzuku bali ni matokeo ya uvumbuzi wa kiteknolojia wa kila wakati na maendeleo yaliyoratibiwa.
Ujumbe huo umesema kuwa China inaweka umuhimu mkubwa sana kwenye sera za biashara na kwamba kwa kutengeneza sera zake za biashara kithabiti, ikiwemo sera za ruzuku, kwa kuendana na kanuni za WTO na mahitaji ya uwazi, China imejitolea kikamilifu kwa mfumo wa biashara wa pande nyingi.
Ujumbe huo umebainisha kuwa kodi ya "kutozana kwa usawa" ya Marekani inavuruga biashara ya kimataifa na kupuuza maslahi ya nchi wanachama zinazoendelea, ukiongeza kuwa China inatuliza biashara ya kimataifa na inasimama imara kwenye upande wa nchi zingine wanachama zinazoendelea.
Ujumbe huo pia umeonesha kuwa sababu ya Marekani kuendelea kuituhumu na kuipaka matope China kuhusu suala la uwezo wa uzalishaji na kuonesha taswira ya China kama “tishio” ni rahisi: Washington muda wote imekuwa ikishikilia mtazamo wa “maslahi ya upande mmoja” na sera ya “Marekani Kwanza”, isiyoamini katika matokeo yenye manufaa kwa pande zote kupitia ushirikiano wa kimataifa.
Aidha, China imekosoa vikali Sheria ya CHIPS na Sayansi ya Marekani na kodi yake ya “kutozana kwa usawa” kwa kuvuruga soko la kimataifa na kukiuka kanuni za WTO. Ujumbe huo umesema kuwa vitendo hivyo vya Marekani si tu vinakiuka sheria za msingi za uchumi wa soko bali pia vinavuruga kwa kiasi kikubwa utaratibu wa biashara na uwekezaji wa kimataifa.
Upande wa China pia umehimiza nchi wanachama wa WTO kuimarisha ushirikiano, kupinga ukandamizaji wa upande mmoja wa Marekani, na kwa pamoja kulinda mfumo wa biashara wa pande nyingi unaozingatia kanuni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma