Russia yatambua "nchi huru" mbili Donbass Mashariki mwa Ukraine huku UN, Marekani na EU zikipinga vikali

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 22, 2022

Rais wa Russia Vladimir Putin akisaini nyaraka za kutambua "Jamhuri wa Watu wa Donetsk na Jamhuri ya watu wa Lugansk" katika Ikulu ya Kremlin mjini Moscow mnamo Februari 21, 2022. (Taarifa ya Kremlin kwa vyombo vya habari)

MOSCOW - Rais wa Russia Vladimir Putin amesaini amri mbili za kutambua "Jamhuri ya Watu wa Lugansk (LPR)" na "Jamhuri ya Watu wa Donetsk (DPR)" kama nchi huru na zenye mamlaka kamili.

Katika hafla iliyofanyika Jumatatu kwenye Ikulu ya Russia, Kremlin, Rais Putin na wakuu wa "jamhuri" hizo mbili pia wametia saini Mkataba wa Urafiki, Ushirikiano na kusaidiana kati ya Russia na LPR na DPR.

"Ninaona ni muhimu kufanya uamuzi uliochelewa -- kutambua mara moja uhuru na mamlaka ya DPR na LPR," Putin amesema katika hotuba yake kwa taifa.

"Russia imefanya kila kitu kulinda ukamilifu wa ardhi ya Ukraine" kwa kupigania kutekelezwa kwa Mkataba wa Minsk wa Mwaka 2015, lakini juhudi zote ziliishia bure, Putin amesema.

Kwa mujibu wa Putin, karibu kila siku kuna makombora yanayofyatuliwa kutoka Ukraine yakilenga makazi huko Donbass na "hakuna dalili za kukoma."

Putin amesisitiza kwamba, mgogoro wa kiusalama wa Ulaya umetokea kutokana na upanuzi wa Mashariki wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO), ambayo imesababisha Russia kupoteza imani.

Amesema kuwa ni "suala la muda" tu kwa NATO kukubali Ukraine kuwa nchi mwanachama na kisha kujenga vifaa vya kijeshi katika ardhi yake ili kiwango cha vitisho vya kijeshi dhidi ya Russia viweze kuongezeka kwa kasi.

Putin amebainisha kwamba, wakati Russia ilipozitaka Marekani na NATO zitoe dhamana ya kiusalama, nchi za Magharibi zilipuuza kwa hakika masuala ya kimsingi ya usalama ya Russia na hakuna kilichobadilika katika msimamo wao.

Kutokana na hali hiyo, Russia "ina haki ya kuchukua hatua za kulipiza kisasi ili kuhakikisha usalama wake," Rais Putin amesema.

Putin amesema anafahamu kuwa nchi za Magharibi zinajaribu "kutishia" Russia tena kwa vikwazo, lakini anaamini kuwa vikwazo vitaendelea kwa sababu tu Russia ipo, bila kujali hali ya Ukraine.

Baada ya kutambua uhuru wa LPR na DPR, Putin ameagiza vikosi vya jeshi la Russia kuhakikisha amani katika "nchi" hizo mbili.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kremlin, Jumatatu jioni, Putin alikuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ambao "walionesha kusikitishwa kwao" na mpango wa Putin wa kutambua LPR na DPR, lakini wakati huo huo walionesha utayari wa kuendelea na mawasiliano.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumatatu jioni alielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya uamuzi wa Russia kuhusu hadhi ya Donetsk na Lugansk ya Ukraine.

"Katibu mkuu anachukulia uamuzi wa Russia kuwa ukiukaji wa ukamilifu wa ardhi na mamlaka ya Ukraine na hauendani na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa," imesema taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa UN Stephane Dujarric.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya (EU) wamesema Jumatatu ya wiki hii kuwa umoja huo utachukua hatua za kuwawekea vikwazo wale wanaohusika na Russia kutambua sehemu mbili za Mashariki mwa Ukraine za Lugansk na Donetsk kama nchi huru.

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen walisema "Hatua hii ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na pia mikataba ya Minsk," "Umoja huo utachukua hatua za vikwazo dhidi ya wale waliohusika katika kitendo hiki haramu.”

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House, Jen Psaki amesema Rais wa Marekani Joe Biden hivi karibuni atatia saini amri ya utendaji inayowapiga marufuku Wamarekani kufanya biashara katika sehemu hizo mbili ya Ukraine ambazo Russia imetangaza kuzitambua kama nchi huru.

"Rais Biden hivi karibuni atatoa Amri ya Utendaji ambayo itakataza uwekezaji mpya, biashara na ufadhili wa watu wa Marekani kwenda, kutoka, au katika kile kinachoitwa DNR na LNR ya Ukraine," Psaki amesema katika taarifa hiyo.

"Amri hiyo pia itatoa mamlaka ya kuweka vikwazo kwa mtu yeyote aliyedhamiria kufanya kazi katika maeneo hayo ya Ukraine," amesema Psaki.

"Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Fedha zitatoa maelezo ya ziada hivi karibuni. Pia hivi karibuni tutatangaza hatua za ziada zinazohusiana na ukiukaji wa leo wa wazi wa ahadi za kimataifa za Russia." 

Picha iliyopigwa Februari 21, 2022 ikionesha televisheni inayomwonesha Rais wa Russia Vladimir Putin akizungumza wakati wa hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni mjini Moscow, Russia. (Xinhua/Bai Xueqi)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha